Ahmad Abu Hiba, mkurugenzi wa Kituo cha Uchapishaji cha Furqaan huko Chicago, alisema, "Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, idadi ya maagizo ya uchapishaji wa Qur'ani kwa taasisi yetu imefikia makumi ya maelfu kwa mwezi," ameiambia Al Jazeera.
Akisisitiza kwamba hajakuza idadi hii, aliongeza kwamba, "Ninaweza kuthibitisha hili kwa data na takwimu. Kwa mfano, Novemba 2020, tulikuwa na wastani wa maombi 300 hadi 400 kwa mwezi. Hata hivyo, Novemba 2023, tulipokea maombi 3,600 ya uchapishaji nakala za Qur’ani Tukufu katika mwezi mmoja, na wakati wa Ramadhani iliyopita, mahitaji haya yaliongezeka hadi makumi ya maelfu ya nakala."
Ahmad Abu Hiba pia amebainisha kuwa idadi ya watu wanaosilimu imeongezeka kwa kiasi kikubwa. “Hii kwa kiasi kikubwa inatokana na subira na imani ya watu wa Gaza na uhusiano wao na Qur’ani. Inawavutia Waamerika kuelewa ni ujumbe gani ulio katika Qur’ani ambao unahamasisha uthabiti kama huo."
Amebainisha kuwa, Wamarekani wamevutiwa na subira na uthabiti wa wananchi wa Palestina, jambo ambalo hawajawahi kukutana nalo kabla. “Waislamu katika Palestina wanathamini sana suala la kifo cha kishahidi; mama akimkumbatia mwanawe shahidi, akiwa na ishara za furaha usoni mwake, akimtia moyo kila mtu asilie. Haya ni matukio ambayo raia wa Marekani hawajawahi kuona hapo awali."
Abu Hiba ameongeza kuwa kituo hicho kimekuwa kikifanya kazi huko Chicago, Illinois, kwa miaka 20, kikitoa tafsiri za Qur'ani kwa Kiingereza na Kihispania.
Pia alibainisha kuwa nakala za Qur’ani hutolewa bila malipo kwa wasiokuwa Waislamu ambao wanataka kujifunza zaidi kuhusu mafundisho yake.
IQNA